We capture your memories forever.

Wednesday, October 25

SEKTA BINAFSI YATAKIWA KUPELEKA CHANGAMOTO ZAO SERIKALINI





Sekta Binafsi imetakiwa kuwasiliana moja kwa moja na Serikali ili kutatua changamoto zinazoikabili badala ya kupitia wadau wa nje kwanza, kwa kuwa mlango wa Serikali uko wazi kwa ajili ya majadiliano na kutatua matatizo ya Sekta hiyo.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) katika Mkutano na Sekta Binafsi nchini (TPSF), Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mpango amesema kuwa ni vema Sekta Binafsi ikashirikiana na Sekta ya Umma kwa kuwa zote zinategemeana na hakuna nchi iliyoendelea bila kuwa na Sekta Binafsi ambayo ni imara.
“Sekta Binafsi na Sekta ya Umma hazina budi kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu, tena kwa kuaminiana kwa faida ya Sekta zote mbili na kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla” aliongeza Dkt. Mpango.
Amesema kuwa, lengo la pande zote mbili ni kuharakisha utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuongeza fursa za ajira, kipato cha mwananchi na kuondokana na umasikini uliokithiri kwa kujenga Tanzania inayoongozwa na uchumi wa Viwanda.
Dkt. Mpango alifafanua kuwa Serikali imeendelea kuyafanyia kazi mapendekezo mengi yaliyotolewa na Sekta Binafsi ikiwemo katika kuboresha mazingira ya biashara nchini ikiwemo kuondoa baadhi ya kodi zilizokuwa kero kwa wafanyabiashara.
Baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni pamoja na Serikali kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kumpa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Fedha mamlaka ya kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani bila kuhusisha utaratibu wa kulipa kwanza Kodi ya Ongezeko la Thamani na baadaye kuomba kurejeshewa (Refund) kwenye miradi inayofadhiliwa na wadau wa maendeleo (Grants) au mikopo yenye masharti nafuu (Concessional Loans) ambayo mikataba husika ina masharti ya kutoa msamaha wa kodi hiyo.
“Hatua hii itawezesha wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini kutopata tena usumbufu katika kutekeleza miradi hiyo na miradi kutekelezwa kwa muda uliopangwa” alisema Dkt. Mpango
Ili kuvutia uwekezaji katika sekta za viwanda, kilimo cha mazao na mifugo nchini, Serikali imesamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye bidhaa za mtaji (capital goods) za viwanda vya mafuta ya kula, nguo, ngozi, madawa ya binadamu na mifugo ili kupunguza gharama za ununuzi/uagizaji wa mashine na mitambo watakayonunua wawekezaji kwa ajili ya kusindika na kutengeneza bidhaa mbalimbali.
“Serikali sasa inatoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia sifuri katika huduma zinazotolewa kwenye usafirishaji wa bidhaa/mizigo nje ya nchi (ancillary transport services), hatua itayopunguza gharama za usafirishaji katika bandari zetu na kuifanya Tanzania kuwa njia bora zaidi ya kupitisha bidhaa zinazotoka nje ya nchi kwenda nchi nyingine hususan zisizo na bandari.
Kwa upande wa hali ya Uchumi, Waziri Mpango amesema kuwa robo ya kwanza ya mwaka 2017, uchumi ulikua kwa asilimia 5.7, robo ya pili ulikua kwa asilimia 7.8, hivyo kufanya nusu ya kwanza uchumi kukua kwa asilimia 6.8.
Baadhi ya shughuli za kiuchumi zilizokuwa kwa kasi ni usafirishaji na uhifadhi wa mizigo ambao umekua kwa asilimia 19.8, uchimbaji madini na mawe asilimia 18.0, uzalishaji viwandani asilimia 9.3 na ujenzi asilimia 8.8.
Dkt. Mpango alisema Sekta ya Benki kwa ujumla imeendelea kuwa imara ikiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha juu ya viwango vinavyokubalika kisheria. Kwa kipindi cha mwaka 2009 hadi 2017 huduma jumuishi za fedha zimeongezeka kutoka asilimia 15.8 hadi asilimia 65.3. Upatikanaji wa huduma za kifedha umeongezeka kutoka asilimia 29 kwa mwaka 2009 hadi asilimia 86 kwa mwaka 2017.
Aidha kwa upande wa mikopo kwa Sekta Binafsi ilipungua kutokana na Benki kuchukua tahadhari kutokana na kuongezeka kwa mikopo chechefu (Non-performing loans) ambapo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilichukua hatua kwa kupunguza kiwango cha amana ambacho benki za biashara zinatakiwa kuhifadhi Benki Kuu kama dhamana kutoka asilimia 10 hadi asilimia 8 na riba za mikopo ya benki hizo kushuka kutoka asilimia 16 hadi 12.
Naye mwenyekiti mwenza wa Mkutano huo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage (Mb) amesema kuwa njia bora ya kutatua matatizo ya Sekta Binafsi ni kuendelea kufanyika kwa majadiliano yenye tija.
Mmoja wa wajumbe wa Mkutano huo wa wafanyabiashara ambaye ni wakili wa kujitegemea Bi. Eve Hawa Sinare amesema kuwa ni vema kuangalia mfumo mzuri wa kuweka riba unaofanywa na Benki za biashara ili kuwa na uwiano mzuri.
Vilevile Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Bw. Salum Shamte ameishukuru Serikali kwa kuonesha nia ya dhati ya kushirikiana na Sekta hiyo kwa lengo la kufanikisha ukuaji wa uchiumi wa Viwanda.
Waziri mpango amewahakikishia wafanyabiashara kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kuna majadiliano ya mara kwa mara na wadau hao ili kutatua changamoto zao na pia ameahidi kuandaa Mkutano mwingine ambao utajikita katika masuala ya kodi kabla ya Sekta Binafsi kuwasilisha mapendekezo ya kodi.
Mkutano huo wa Sekta Binafsi na Umma ni wa pili kufanyika, kwa mara ya kwanza Mkutano kama huo ulifanyika tarehe 11 Aprili, 2017 mjini Dodoma ambapo ulisaidia kutatua changamoto nyingi ikiwemo kusaidia kuongezeka kwa ufanisi katika huduma za bandari nchini.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Godfrey Simbeye akifafanua jambo kwa wafanyabiashara waliohudhuria katika Mkutano kati yao na Serikali uliolenga kujadili mafanikio na changamoto za pande hizo mbili, uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti mweza wa mkutano kati ya Serikali na Sekta Binafsi, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage akielezea kuhusu umuhimu wa majadiliano katika kutatua changamoto za kibiashara nchini, mkutano uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akizungumza na wafanyabiashara Jijini Dar es Salaam kuhusu umuhimu wa kupeleka taarifa za changamoto zao Serikalini ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kulia) akifuatilia majadiliano kati ya Sekta Binafsi na ya Umma yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam lengo likiwa kutatua changamoto mbalimbali.

Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Mwigulu Nchemba (kulia) na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Walemavu, Mhe. Anthony Mavunde (Mb) wakibadilishana mawazo wakati wa Mkutano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi.

Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Bw. Salum Shamte akishukuru juhudi za Serikali katika kuzileta pamoja Sekta binafsi na ya umma, wakati wa Mkutano kati ya Sekta hizo mbili Jijini Dar es Salaam.






Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akipeana mkono na Mfanyabiashara Mohammed Dewji wakati wa Mkutano kati ya Sekta Binafsi na Umma Jijini Dar es Salaam

Baadi ya Wafanyabiashara Jijini Dar es Salaam wakifuatilia Mkutano kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma uliolenga kutatua changamoto za Sekta hizo ili kuharakisha ukuaji wa uchumi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu (wa pili kushoto) na Kamishna Msaidizi wa Sera kutoka Wizara hiyo Bw. Shogholo Msangi na wafanyabiashara wakifuatilia maelezo kutoka kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani) kuhusu umuhimu wa majadiliano katika kujenga uchumi wenye tija kwa Sekta Binafsi na ya Umma.

Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani (Mb) akizungumza kuhusu namna Serikali ilivyojipanga katika kutatua tatizo la Nishati ya umeme ili kuweza kuchochea uchumi wa Viwanda wakati wa Mkutano kati ya Sekta Binafsi na Umma uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Thursday, October 12

MRADI WA UMEME WA MAKAMBAKO-SONGEA KUNUFAISHA MIJI NA VIJIJI 191







NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, MAKAMBAKO


KUKAMILIKA kwa Mradi wa ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovolti 220kV, na usambazaji umeme vijijini kutoka Makambako-Songea kupitia Njombe, unatarajiwa kuondoa kabisa tatizo la upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi wa mijini na vijiji vipatavyo 191, Meneja wa Mradi huo Mhandisi Didas Liyamuya,(pichani juu), amesema leo Jumanne Oktoba 10, 2017 wakati wa ziara ya Wahariri wa vyombo vya habari nchini.


Sambamba na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme pia utahusisha upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Makambako cha msongo wa umeme wa kilovolti 220/132/33Kv, na ujenzi wa vituo vingine vipya viwili, vya Madaba na Songea vya msongo umeme wa kilovolti 220/33kV, halikadhalika ujenzi wa mfumo wa usambazaji umeme wa msongo wa kilovoti 33 pamoja na kuunganisha wateja 22,700, katika mikoa hiyo alisema Mhandisi Liyamuya.


Akifafanua zaidi, katika mkoa wa Njombe, umeme utasambazwa katika maeneo ya Makambako na viunga vyake, Njombe yenyewe, na Ludewa, wakati mkoa wa Ruvuma umeme utasambazwa katika mji wa Songea na vijiji vilivyo katika wilaya ya Mbinga, Namtumbo na Madaba, na kuongeza kuwa umeme utakuwa wa msongo wa kilovolti 33 pamoja na ujenzi wa mawasiliano “OPGW”.


“Lengo la mradi huu ambao unafadhiliwa na Serikali ya Swedena kupitia Shirika lake la Misaada ya Kimaendeleo SIDA, Serikali ya Tanzania na Shirika la Umeme Nchini, TANESCO, ni kuboresha hali ya upatikanaji umeme katika maeneo ya uzalishaji na majumbani.” Alifafanua.


Wahariri hao walipata fursa ya kutembelea eneo la upanuzi wa kituo cha Makambako ambapo walishuhudia kazi ya kujenga misingi ya mitambo ikiwemo Slope protection. Pia walijionea kazi ya kufunga transfoma kwenye maeneo kadhaa ya Makambako ikiwemo eneo la Lyamkena.Mhandisi Liyamuya alibainisha kuwa awamu ya kwanza ya mradi wa kusambaza umeme utakamilika Desemba 2017 wakati awamu ya pili utakamilika Novemba 2018.


“Hadi leo hii Oktoba 10, 2017, mradi umekamilika kwa asilimia 63 kwa upande wa mkoa wa Ruvuma na asilimia 39.5 kwa upande wa mkoa wa Njombe na kazi kubwa iliyofanyika ni ubainishaji wa maeneo ya kupitisha laini (njia ya umeme), ubunifu wa jinsi muundo wa njia hiyo utakavyokuwa, ufyekaji wa njia za kupitisha laini, ununuzi wa vifaa pamoja na kusimamisha nguzo za msongo wa 33kV na 400V na kusambaza nyaya, na usimikaji wa Transofa.” Alisema.


Hata hivyo Mhandisi Lyamuya alieleza masikitiko yake kwa baadhi ya watu kuchoma moto ovyo misitu ambapo baadhi ya nguzo zilizosimikwa katika kipindi hiki cha mradi zimeungua.


“Nitoe rai kwa watanzania wenzangu, Serikali inafanya juhudi kubwa kuwafikishia huduma hii muhimu ya umeme, na mfahamu kwamba fedha za walipa kodi wa Tanzania Shilingi Bilioni 7 zilitolewa kama fidia, iweje leo tuanze kufanya uharibifu huo.?” Alihoji, na kutaka vimgozi wa serikali kwenye maeneo yote ya mradi kuwahamasisha wananchi kutunza miundombinu hiyo ambayo inaligharimu taifa fedha nyingi.

Mmoja wa wakazi wa kitongoji cha Lyamkena, mji wa Makambako mkoani Njombe, ambaye ni mteja mpya wa TANESCO, Bw.Thomas Kiwale, (kulia), akihakikiwa wakati wa zoezi la kuwahakiki wateja walioomba kuunganishiwa umeme kwenye eneo hilo, na afisa wa TANESCO, Bi.Atuokoe Mhingi, Oktoba 10, 2017

Wahariri na mafundi wa TANESCO, wakipita chini ya moja ya transofa zinazoednelea kufungwa kwenye mji wa Makambako Oktoba 10, 2017.

Baadhi ya wahariri wakisikiliza maelzo yaliyokuwa yakitolewa na Mhandisi Liyamuya(hayupo pichani), kuhusu utekeelzaji wa mradi huo walipotembelea eneo la upanuzi wa kituo cha kupoza na kusafirisha umeme wa 220kV cha Makambako.

Baadhi ya wahariri na mafundi wa TANESCO, wakisikiliza maelzo yaliyokuwa yakitolewa na Mhandisi Liyamuya(hayupo pichani), kuhusu utekeelzaji wa mradi huo walipotembelea eneo la upanuzi wa kituo cha kupoza na kusafirisha umeme wa 220kV cha Makambako.
Kaimu Meneja Uhusiano wa TANESCO, Bil Leila Muhaji, akifafanua baadhi ya mambo ambapo alisema, ili kujenga uhusiano mwema na wananchi walio jirani na eneo la Mradi, wateja watatozwa kiasi cha shilingi 27,000 tu kwa kazi hiyo katika kipindi hiki cha utekelezaji wa mradi, na hivyo kuwataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya umeme kwa faida ya taifa na wao wenyewe.

Bi.Atuokoe Mhingi,kutoka TANESCO, akiendelea na zoezi la kuwahakiki wateja walioomba kuunganishiwa umeme kwenye eneo la Lyamkena, Makambako Oktoka 10, 2017.

Moja ya minara ya kusafirisha umeme wa 220kV. ambao tayari umejengwa nje kidogo ya mji wa Makambako.

Moja ya minara ya kusafirisha umeme wa 220kV. ambao tayari umejengwa nje kidogo ya mji wa Makambako.

Mhariri wa Mwananchi Online Digital, Peter Nyanje, (kushoto) na Mhariri wa gazeti ka Majira, Bw. Mwafisi wakifurahia jambo.





Mhariri wa gazeti la Nipashe, Bw. Joseph Mwendapole, (kulia), akionyeshwa moja ya minara ya kupitisha umeme wa 220kV nje kidogo ya Makambako.
















Kazi ya ujenzi wa msingi wa kufunga mitambo kwenye eneo la upanuzi wa kituo cha kupoza umeme wa 220kV Makambako ikiendelea.







Kaimu Meneja Uhusiano wa TANESCO, Bi. Leila Muhaji, (kulia) na Afisa Uhusiano wa Shirika hilo, Bi. Grace Kisyombe wakijadiliana jambo.







Meneja Mradi wa ujezni wa njia ya kusafirisha umeme kutoka kampuni ya Isolux,Bw.Elmensour,(kulia), akielezea jinsi kazi hiyo inavyoendelea







Wahariri kutoka kushoto, Peter Nyanje, Joyce Shebe na Nevile Meena

DC ARUSHA MJINI AWATAKA WANANCHI KUJIANDIKISHA VITAMBULISHO VYA TAIFA






Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Fabian Daqqaro amewataka wananchi wa wilaya ya Arusha Mjini Kuchangamkia zoezi la Uandikishwaji Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ambalo linaendelea katika kata tatu za Wilaya hiyo.

Akizungumza katika kipindi cha Goodmorning Tanzania kinachorushwa na kituo cha Matangazo cha Redio cha Redio 5 Arusha Daqqaro, amesema kuwa zoezi hili lina manufaa makubwa kwa wananchi na watanzania kwa ujumla lakini pia vitambulisho hivyo vitawawezesha watanzania kutambulika kila mahala, pamoja na raia wa kigeni kufanya shughuli zao bila usumbufu ikiwa ni pamoja serikali kuwa na taarifa sahihi za wananchi.

Aidha amesema kuwa wananchi wasisubiri mpaka zoezi hilo kufikia tamati ndio kujitokeza Kwa wingi kwa kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha msongamano na usumbufu mkubwa kwa wananchi.

“Naomba niwafahamishe na kutoa rai kwa wananchi wangu wajitokeze kwa wingi katika zoezi hili na wasisibirie siku kubaki chache ndio wajitokeze kwa kuwa kunapelekea usumbufu mkubwa sana hivyo,zoezi hili pia litakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi”alisema fabian


Pia ametaka kila mwananchi kushiriki zoezi hilo na kutolihusisha na masuala ya kisiasa kutokana na umuhimu wake,kwa kuwa lengo ni kutambua na kusajili na kutoa vitambulisho vya taifa.

Afisa kutoka mamlaka hiyo wilaya ya Arusha Mjini Juliette Raymond Amesema lengo la zoezi hilo ni kuwezesha serikali kutambua wananchi wake wapo wapi na wanafanya nini ilimradi anaishi ndani ya mipaka ya Tanzania ,hivyo zoezi hilo ni lazima kwa kila mtu kwa Mujibu wa sheria.

Kwa wilaya ya Arusha Mjini zoezi hilo linaendelea katika kata ya Sombetini,Sekei na Themi ambapo zoezi hilo linafnyika katika Halmashauri ya Jiji la Arusha katika kata ya Sekei,Themi katika viwanja vya nane nane na Sombetini Ofisi za Mtendaji kata eneo la Mbauda Sokoni.

Wednesday, October 11

VIGUTA WAWAPATIA UZALENDO KWANZA VIWANJA, NYUMBA MKOANI PWANI


Mwenyekiti wa Umoja wa Vicoba Tanzania (Viguta) Taifa, Dk. Dauda Salmin (kulia) akishikana mikono na Mwenyekiti wa Uzalendo Kwanza, Steve Nyerere mara baada ya kusaini mkataba wa ushirikiano ya kufanyakazi pamoja ambapo UZALENDO KWANZA NA VIGUTA watakuwa bega kwa bega kutoa elimu ya ujasiliamali Tanzania nzima katika hafla iliyofanyika jana Kijiji Cha Kwala - Chalinze. Mwenyekiti wa Umoja wa Vicoba Tanzania (Viguta) Taifa, Dk. Dauda Salmin (kulia) wakisainisha mkataba wa ushirikiano na Mwenyekiti wa Uzalendo Kwanza, Steve Nyerere ili kuendelea kutoa elimu ya ujasiliamali Tanzania nzima katika hafla iliyofanyika jana Kijiji Cha Kwala - Chalinze.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vicoba Tanzania (Viguta) Taifa, Dk. Dauda Salmin (kulia) akipongezana na Mwenyekiti wa Uzalendo Kwanza, Steve Nyerere mara baada ya kumaliza kusaini makubaliano.


Salamu za pongezi zikiendelea kutolewa mara baada ya kumaliza zoezi la kusaini mkataba. Mbunge wa viti maalum wa Pwani, Hawa Mchafu Chakoma (CCM) ambaye alikuwa mgeni rasmi akitoa neno kwa wasanii na wananchi walihudhuria hafla hiyo. Mwenyekiti wa Umoja wa Vicoba Tanzania (Viguta) Taifa, Dk. Dauda Salmin akiwatambulisha wanachama


Mwenyekiti wa Uzalendo Kwanza, Steve Nyerere akitoa neno la shukrani mara baada ya kusaini mkataba wa ushirikino wa kufanya kazi pamoja. Pia aliwashukuru kwa kuweza kuwapatia viwanja kwa ajili ya kujenga nyumba zao za kuishi. Hafla hiyo ilifanyika jana Kijiji Cha Kwala - Chalinze.

Mbunge wa viti maalum wa Pwani, Hawa Mchafu Chakoma (CCM)




Wananchama wa Viguta na Uzalendo Kwanza wafuatilia halfa hiyi.

Wanachama wa Uzalendo Kwanza na Viguta wakielekea eneo la viwanja walivyopewa.

Mwenyekiti wa Uzalendo Kwanza, Steve Nyerere akikabidhiwa nyumba na Mbunge wa viti maalum wa Pwani, Hawa Mchafu Chakoma (CCM) ambaye alikuwa mgeni rasmi katika halfa ya ushirikiano na Viguta.


Mwenyekiti wa Uzalendo Kwanza akionyesha mkataba wa nyumba aliyopewa na Viguta.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vicoba Tanzania (Viguta) Taifa, Dk. Dauda Salmin akikabidhiwa nyumba na Mbunge wa viti maalum wa Pwani, Hawa Mchafu Chakoma (CCM) ambaye alikuwa mgeni rasmi katika halfa ya ushirikiano na Viguta.

Moja ya nyumba aliyopewa mwenyekiti wa Uzalendo Kwanza, Steve Nyerere na Viguta.


Burudani ikitolewa.