We capture your memories forever.

Thursday, July 27

URIO CUP YAZINDULIWA RASMI DAR





Mashindano ya mpira wa Miguu maarufu kama URIO CUP 2017 yamezinduliwa rasmi Jijini Dar es Salaam. Mashindano hayo, yanayoratibiwa na Msonge Africa Kwa kushirikiana na Jomo International na kudhaminiwa na Times FM, yana lengo la kuzikutanisha timu 32 zinazotokea katika sehemu mbalimbali za Mkoa wa Dar es Salaam ili kuleta hamasa katika kata ya Kunduchi na pia kuzipa timu za kata hiyo uzoefu.


Akizindua mashindano hayo, Diwani wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio ambaye ndio mdhamini na mwanzilishi wa kombe hilo la Urio Cup alisema hii ni mara ya pili kwa mashindano hayo kufanyika kwani mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2015 na kuhusisha timu 16 na kuongeza kuwa Urio Cup mwaka huu inaenda sambamba na Kampeni maalumu ya ‘Wezesha Mama na mtoto Mpya wa Kuncuchi’ ambayo ilizinduliwa hivi karibuni na yenye lengo la kuboresha zahanati ya Ununio na Mtongani. Diwani wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio akipiga danadana ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Urio Cup mashindano ambayo yanatarajiwa kufanyika katika kata yake kuanzia mwezi ujao. Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Radio Times FM, Rehure Nyaulawa, Mratibu wa Urio Cup, Deus Buhilo na Katibu wa Ligi na Mashindano wa Chama Cha Mpira Wilaya ya Kinondoni, Khalid Shehani.


“Moja ya ahadi nilizotoa kwa wananchi wangu ni kuimarisha sanaa na michezo kwani michezo sasa hivi ni chanzo kikubwa cha ajira hasa kwa vijana. Urio Cup iliyopita ilitoa baadhi ya wachezaji waliojiunga na timu za daraja la kwanza na nimefahamishwa kuwa kuna wengine pia wanacheza ligi kuu,” alisema Mh. Urio.


Alitoa wito kwa wadau mbalimbali wapenda michezo wamuunge mkono katika hili ili kombe hili liweze kukua mwaka hadi mwaka na kuwafadisha vijana wengi zaidi. “Nimearifiwa kuwa tutawaalika wawakilishi kutoka timu za ligi kuu ili waweze kutafuta vipaji kutoka kwa timu zitakazoshiriki Urio Cup.


Hili litasaidia sana katika kuamsha ari ya vijana huku wote wakiwa na matumaini ya kusajiliwa na timu kubwa siku moja,” alisema diwani huyo. Naye mratibu wa Urio Cup, Bw. Deus Buhilo alisema maandalizi yote yamekamilika na wanatarajia kushindanisha timu 32 ambazo zinatakiwa kujisajili na kulipia ada ya Tsh 70,000 na timu zinazotakiwa kujisajili zinatakiwa kutuma maombi na kupata maelekezo kupitia namba 0652559122 na malipo kupitia namba 0628555333.

Diwani wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio akizungumza wakati wa uzinduzi wa Urio Cup mashindano ambayo yanatarajiwa kufanyika katika kata yake kuanzia mwezi ujao. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Radio Times FM, Rehure Nyaulawa na Katibu wa Ligi na Mashindano wa Chama Cha Mpira Wilaya ya Kinondoni, Khalid Shehani.


“Urio Cup ni mashindano makubwa na tumeweka vigezo ili kuhakikisha tunakuwa na mashindano bora yanayofuata kanuni zote za FIFA na TFF. Tunataka kuwajengea vijana wetu uzoefu ili waweze kufika katika ngazi za juu zaidi,” alisema mratibu huyo na kumshukuru Diwani Urio kwa kuanzisha mashindano hayo.


Alisema mechi zitachezwa katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Tegeta na zitaanza katika hatua ya mtoano nyumbani na ugenini na mshindi ndiye ataendelea katika hatua inayofuata huku fainali za mashindano hayo yakifanyika Katika Uwanja wa Machava uliopo Kunduchi Beach ambao kwa sasa umeanza kufanyiwa matengenezo.


Alisema mshindi wa kwanza atajinyakulia Tsh 3,000,000 na kombe, wa pili 1,500,000, timu yenye nidhamu Tsh 100,000, mfungaji bora Tsh 100,000, Kikundi bora cha ushangiliaji Tsh 100,000, kipa bora Tsh 100,000 na mchezaji bora (man of the match) Tsh 10,000 na kuongeza kuwa timu zitakazotinga katika hatua ya 16 bora zitapata jezi.


“Mashindano haya yatafanyika kwa miezi mitatu kuanzia Agosti 7 na tunatoa wito kwa timu mbalimbali zijitokeze kujisajili na wakazi wa Dar es Salaam wajitokeze kwa wingi pia kufuatilia,” alisema huku akiongeza kuwa kiingilio katika kila mechi ni Tsh 500 ili kuhamasisha watu wengi zaidi kupata nafasi ya kutazama mashindano hayo. Naye Katibu wa Kamati ya Ligi na Mashindano wa Chama Cha Mpira Wilaya ya Kinondoni (KIFA), Khalid Shehani alitoa pongezi kwa Diwani Urio kwa juhudi zake za kukuza mpira katika kata yake na kumhakikishia ushirikiano mkubwa. “Hii ni hatua kubwa mno na TFF inaunga mkono hatua hizi asilimia 100 na tutatoa ushirikiano mkubwa ili kwa pamoja tuendeleze mpira wetu.


Timu zitakazoshiriki zijiandae vizuri na kuyapa mashindano haya umuhimu mkubwa kwani ni ngazi ya kufika katika hatua nyingine za juu zaidi,” alisema na kuomba timu zitakazoshiriki kuzingatia kanuni na taratibu zote za mpira ili kuepukana na matatizo.

No comments:

Post a Comment